Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kuruhusu Shirika la umeme nchini TANESCO kupandisha gharama za umeme kwa asilimia 18.5 kuanzia Januari 2011 na kweli imekuwa hivyo.
Katika kuhalalisha ongezeko hilo, EWURA wamesema kuwa TANESCO walikuwa wameomba kupandisha gharama za umeme kwa asilimia 34.6 kuanzia Januari mwakani lakini wao EWURA baada ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusiana na maombi hayo wameamua kuwaruhusu TANESCO kupandisha umeme kwa hizo asilimia 18.5 tu ikiwa ni zaidi kidogo ya nusu ya kile walichokuwa wameomba TANESCO.
Tukumbuke kuwa miaka mitatu iliyopita TANESCO pia iliwasilisha maombi EWURA kutaka kuruhusiwa kupandisha gharama za umeme kwa 40% lakini mamlaka hiyo baada upembuzi yakinifu mwingine iliiruhusu TANESCO kupandisha umeme kwa asilimia 21.7 ambayo pia ni zaidi kidogo ya nusu ya kile walichoomba TANESCO.
Haingii akilini wateja kuanza kukamuliwa ongezeko la gharama la asilimia 18.5 huku ukosefu wa nishati hiyo muhimu ukiwaathiri kwenye shughuli zao za kujitafutia kipato. Huku ni sawa na kutaka kumkamua ng’ombe kilasiku bila kumpa majani.
Katika hotuba yake ya kufunga mwaka, Rais Jakaya Kikwete aliwasihi Watanzania kukubaliana na ongezeko hilo la gharama za umeme kutokana na gharama kubwa zinazoikabili TANESCO katika kuzalisha nishati hiyo muhimu.
Rais Kikwete pia alitetea upandaji huo wa gharama za umeme kwa asilimia 18.5 kwa maelezo kuwa ulikuwa umepita muda mrefu, miaka minne, tokea TANESCO wapandishe gharama za umeme kwa mara ya mwisho. Swali langu ni je, ipite miaka mingapi tena gharama za umeme zipande kufikia kiasi gani? Kwa sababu rais kadhihilisha ili yawe maisha bora kwa kila mtanzania.
Je, Serikali iko tayari kuwachukulia hatua watendaji wake wote ambao kwa namna moja ama nyingine wameshiriki kuiingiza TANESCO, na Watanzania, kwenye mikataba ya giza?
Miktaba inayolikamua taifa kuanzia IPTL hadi sasa ambapo mwaka huu tunauanza kwa balaa la kutakiwa kulipa watu hao shilingi Bilioni 185 licha ya kwamba hawajatuuzia chochote!
Kwa hakika ni kejeli, watawala wetu wanapodai kuwa haya ni “maisha bora kwa kila Mtanzania” wakati shirika la kusambaza umeme la taifa linalazimika kumkamua mwananchi zaidi ya shilingi milioni mbili pale anapotaka kuingiza umeme kwenye kibanda chake panapohitajika nguzo moja tu, kwa vile tu Shirika linahitaji hela hizo sio kwa ajili ya kuboresha huduma zake bali kwa ajili ya kulipa madeni!
Inashangaza jinsi wataalamu wetu wanavyotetea kupanda kwa gharama za umeme za hapa nyumbani kwa kujilinganisha na nchi nyingine zilizopo kwenye ukanda wetu wa Afrika Mashariki bila kutufahamisha kuhusu tofauti kubwa iliyopo kati ya uchumi wetu na ule wa nchi hizo.
Ni kitu cha ajabu sana kwamba kwa kipindi cha zaidi ya miaka 15 kuanzia pale tulipoanza kuhangaika upungufu wa nishati ya umeme bado watawala wetu wameshindwa kupata ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo linaloumiza uchumi wa nchi na wa wananchi wake.
Kwa hakika ni kichekesho cha aina yake ambacho kinawezekana Tanzania tu cha kulipa mabilioni ya fedha zetu za ngama kwa makampuni hewa ya kufua umeme hewa ambayo yanamilikiwa na wamiliki hewa huku tukiendelea kuwa gizani!
Jambo la ajabu zaidi ni kwamba wakati watawala wetu wanadai kwamba nchi yetu haina uwezo wala fedha kwa ajili ya kutoa elimu ya bure kwa watoto wetu, bado nchi ina uwezo wa kulipa mabilioni ya shilingi kwa makampuni hewa kwa ajili ya kununua giza letu wenyewe!
Serikali pia hung’aka kwa kauli kali na za vitisho linapokuja suala la kuongeza mishahara ya wafanyakazi wake na malipo mbali mbali ambayo yangeweza kuwapa unafuu wa maisha wananchi wake kama vile yale ya wastaafu wa iliyokuwa jumuiya ya Afrika Mashariki na kati, na wahdhili wa chuo kikuu cha Dodoma, ukali huo hutoweka pale linapokuja suala la kulipa makampuni yaliyotuuzia umeme hewa.
Nchi hii imejawa na makaa ya mawe mengi tu kwa mfano; Kiwira-Mbeya, gesi pia kusini mwa tanzania ipo ya kutosha kabisa, lakini cha ajabu tumeruhusu watu wamejimilikisha kwa bei waipendayo wao na kuzalisha pato lisilo na mchango wowote hapa nchini. Kwanini tusiwataifishe na kuanza kuchimba makaa ya mawe na gesi kwa kuzalisha nishati yetu hapa nchini? Au kama inashindikana basi serikali iibinafsishe TANESCO.
Maisha ya watanzania yanazidi kuwa mabovu kila kukicha afadhali ya Jana, hii ni kwasababu unapopandisha umeme unavifanya viwanda vizalishe kwa garama ya juu. mafuta ya petrol,diesel, na ya taa vile vile yatapanda bei, usafiri lazima bei iende juu, vyakula navyo vitapanda bei maana vinahitaji kusafilishwa toka vijijini (mashambani) kuingia mitini. Je, haya ndiyo maisha bora kwa kila mtanzania?
Maoni yangu ni kwamba, ifike pahala tuchachamae sasa, tuseme hapana. Hivi tujiulize, ni kesi gani serikali yetu ya Tanzania ilishasimamia kesi na kushinda? Jibu litakuja ni hapana. Na je, kama kweli wamiliki wa dowans ni halali kwanini walikuwa hawajulikani? Jamani, hizo bilioni 185 zingetosha kulipia wanafunzi wote vyuo vikuu vyote (30) hapa nchini kila mwanafunzi akapata 100% kwa miaka yote mitatu kuliko ilivyo hivisasa.
Mwisho mimi kama raia wa hii nchi (victim) nasema hivi, waziri Ngeleja kwa namna moja au nyingine zaidi Mafisadi wamekutuma kuutangazia uma uongo, tambua kuwa umejishushia heshima kwa watanzania. Imani juu yako sasa haipo tena, unapaswa kujiuzulu kwa maslahi ya Taifa. Wamiliki wa DOWANS wanafahamika kwa mujibu wa spika mstaafu, mheshimiwa sana Samwel Sita, na wamekithili kwa ufisadi. Hizo pesa kulipwa ni hadi wafilisiwe wote waliohusika katika hiyo mikataba zikitosha deni ndipo zitumike kulipa.
No comments:
Post a Comment