Polisi wamewaua watu wawili kwa kuwapiga risasi na kuwajeruhi wengine tisa, katika harakati za kudhibiti maandamano ya amani yaliyofanywa na wafuasi wa Chadema juzi mkoani Arusha.
Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Thobias Andegenye jana aliwataja waliouawa katika tukio hilo kuwa ni Denis Michael Shirima (25) ambaye ni mmiliki wa gereji ya magari katika eneo la Sakina na George Mwita Waitara (24), mkazi wa Sakina mkoani humo.
Hata hivyo habari ambazo Mwananchi lilizipata zinasema kuwa watu waliouwawa katika vurugu hizo ni watatu, kufuatia kifo cha mtu aliyetajwa kwa jina la Ismail Omar.
“Watu hawa waliuawa kwa kupigwa risasi katika vurugu, Shirima alipigwa tumboni na Waitara ubavuni,”alisema Andengenye.
Kwa mujibu wa kamanda Andengenye, watu sita walijeruhiwa kwa kupigwa risasi sehemu mbali mbali za miili yao , huku polisi wawili wakijeruhiwa katika maandamano ya juzi jioni.
“Hali za polisi zinaendelea vizuri na wanapatiwa matibabu sambamba na wananchi wengine. Tunaomba amani Arusha,”alisema Andengenye.
Hata hivyo wakati polisi wakiripoti kuwauwa watu wawili, habari zilizoenea mkoani Arusha na mikoa ya jirani zinadai kwamba watu waliokufa katika mapambano hayo ni zaidi ya kumi.
Kamanda Andengenye alisema vurugu hizo zilizodumu kutwa nzima juzi na jana asubuhi, zilisababisha uharibifu mkubwa wa mali , likiwemo jengo la mfanyabiashara, Salimu Ally ambalo lilichomwa moto.
Uharibifu mwingine ulifanyika katika vituo vya polisi vya Unga Limited na Kaloleni.
“Kituo chetu cha polisi Kaloleni kimenusurika kuchomwa moto, kuna vibanda vya simu vimechomwa moto, jengo la CCM limevunjwa vioo lakini nalo, lilikuwa lichomwe moto,”alisema Kamanda Andengenye.
Katika hatua nyingine, Andegenye alitangaza kukamatwa kwa watu 49 wakiwemo viongozi wanane wa Chadema, kutokana na vurugu za maandamano ya hiari ya yaliyofanywa na chama hicho juzi.
Baadaye jana jioni watu 31 kati ya hao walifikishwa mahakamani.
Taarifa ya Andegenye ilikuja wakati kukiwa na taarifa za kusakwa viongozi wa Chadema mkoa wa Arusha kutokana na vurugu hizo.
Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, alithibitisha jana kusakwa na polisi na viongozi wenzake kadhaa.
“Mimi na wenzangu wanatutafuta tangu jana usiku…imebidi kujificha ili kuwezesha masuala ya dhamana ya viongozi wa kitaifa,”alisema Mwigamba.
Viongozi hao, wanatuhumiwa kutoa kauli za uchochezi katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya NMC juzi.
Habari hii imeandaliwa na Mussa Juma na Moses Mashala, Arusha na Felix Mwagara na kuletwa kwenu na Aloyce kalunde, ikiwa imechotwa nzimanzima kama ilivyo kutoka:
Source: http://dullonet.com/2011/01/07/igp-mwema-akiri-polisi-wake-kuua-kwa-risasi-arusha/on 07thjanuary,2011.
No comments:
Post a Comment