Ansbert Ngurumo
WASOMAJI kadhaa wameniomba niwakumbushe hoja niliyoandika Desemba 23, 2007 nilipohoji, “kwanini tuchague jiwe?” Wanadai kwamba mjadala wa kisiasa uliotawala nchini wiki hii unafanana na hoja yangu ya miaka miwili iliyopita.Ingawa baadhi ya matukio yanayosimuliwa katika makala ile yalikwisha kubadilika, nimeona vema nikubali ombi la baadhi ya wasomaji wa Maswali Magumu, niiweke kama ilivyokuwa, itumike kama fursa ya kupima na kujipima kama katika miaka miwili iliyopita tumesonga mbele, tumerudi nyuma au tumegota pale pale. Wakati ule, niliandika hivi:
Mtu mmoja ameingia kwenye blogu yangu (www.ngurumo.blogspot.com) kujadili mapinduzi niliyopendekeza, akaandika maoni yake, ambayo nimeona yawe sehemu ndogo (lakini muhimu) ya mjadala wa leo. Alificha jina lake, akaandika hivi:
“Mapinduzi ya kweli mpaka tupate viongozi wa maana... Nchini bado hakuna viongozi wa maana watakaoleta mapinduzi ya maana.
“Tuna wakosoaji sampuli ya Ngurumo, ana chuki na Kikwete utafikiri walichukuliana mabibi. Nchi hii usanii tu. Wakosoaji wasanii, watawala wasanii, wapinzani wasanii, hakuna lolote; porojo tu...”
Kwa maoni ya mwananchi huyu, Tanzania ni nchi ya wasanii; yeye akiwamo! Haina uongozi wala upinzani. Haina watu makini na haina kitu. Ni nchi iliyo tupu na ukiwa!
Kwangu, huyu ni mtu aliyekata tamaa. Hana tumaini lolote. Uwezo wake wa kuvumilia adha na kustahimili mapambano ya kila siku umefikia kikomo.
Hatafuti ufumbuzi kwa sababu haoni kama inawezekana. Na anaona watu wanaozungumzia ufumbuzi wa matatizo ya kitaifa wanaota ndoto za mchana.
Watu wa namna hii ndio huishia kujinyonga; maana hawaoni haja ya kuishi; na hata wao wenyewe hawaamini kwamba wapo hai!
Ingawa hii imejitokeza kwenye blogu, ambako nilidhani wananchi wengi wasio na mtandao wa kompyuta hawatapata fursa ya kuisoma, nimekuwa napata kauli za namna hii kutoka kwa baadhi ya watu ninaowafahamu walio serikalini.
Kama jamaa huyu, nao hawana imani na serikali inayowaajiri. Hawana imani na wanasiasa wanaoongoza serikali wala upinzani unaoikosoa serikali. Wanafanya kazi kwa kutimiza tu wajibu, lakini hawana ari!
Je, hawa wanaweza kufanya kazi kwa ufanisi na tija? Mwajiri wao anajua jinsi watu wake walivyokata tamaa?
Hili ni kundi la watu wanaoogopa mijadala, hata ile ambayo ingewasaidia kuinua upya nafsi zao zinazochungulia shimoni. Katika hali ya kukata tamaa, hawasomi hata hoja za wakosoaji na wapinzani wa serikali.
Hata wakizisoma hawaelewi; kwa maana wameshafunga milango ya uelewa. Wanachokiona ni chuki.
Kinachosikitisha ni kwamba hawamtazami rais wetu kama kiongozi; bali kama mwanaume tu ‘mpenda mabibi’ akiwagombea na wananchi wake! Kwa maoni yangu, hii ni dhihaka isiyo kifani dhidi ya viongozi wetu, hata kutoka kwa watu wenye nia ya kumtetea na kuwakatisha tamaa wanaomkosoa.
Ajabu ni kwamba, baadhi ya watu wenye upeo huu, wanaozungumza lugha hizi – walau wale ninaowafahamu – wamejichomeka na kukubalika katika kundi la washauri wa watawala wa nchi hii.
Mawazo ya namna hii yamo serikalini na nje ya serikali. Ni ugonjwa mbaya wa kiakili na ni sehemu ya mambo yanayopaswa kupinduliwa kama tunataka kuiokoa Tanzania.
Ndiyo maana sikukaa kimya, bali nilimjibu kwa kifupi na bila kuchuja maneno, pale pale kwenye blogu. Nilimjibu hivi:
“Mimi siandiki kwa upendeleo wala woga. Naandika kile ambacho mashabiki wa (Rais Jakaya) Kikwete hawataki kukiandika kwa sababu wanaona ‘watamharibia.’
Mimi nalitazama taifa si CCM. CCM imekaa madarakani miaka nenda rudi. Imechoka. Imeishiwa mikakati. Inarudiarudia yale yale. Tunaisahihisha kwa nia ya kujenga nchi - na kuwasaidia kuamka usingizini.
Kwa nini Kikwete? Ndiye rais wetu. Ana mamlaka makubwa mno kikatiba. Ama yapunguzwe, au ayatumie kujenga nchi, si kushibisha matumbo ya wanaomuunga mkono.
Zaidi ya hayo, kabla hajaingia (madarakani) tuliahidiwa makubwa mno kutoka ‘kwake’. Sasa kama tumegundua ana ‘uwezo’ mdogo, huku akiwa na ‘mamlaka makubwa’ tusiseme?
Naamini kusema huku ni njia nyingine ya kuwaamsha waliolala, kumwamsha naye atumie mamlaka aliyo nayo, na kuwaamsha wasaidizi wake, hata kudai mabadiliko ya katiba ili mambo ya msingi ya kitaifa yafanyike, tusibaki kumtazama na ‘kumwabudu’ mtu mmoja, kiongozi dhaifu tunayemuona malaika - huku nchi inadidimia.
Najua jambo moja. Wanaomtetea Kikwete hawampendi, lakini wanashibia mgongoni mwake; au wana matumaini ya kushiba akiwa pale. Lakini hawamsaidii wala hawalisaidii taifa. Mimi nitamsaidia kwa kumkosoa!”
Ni vema tukumbushane kwamba mapinduzi ya kweli hayaji kwa nguvu ya viongozi, bali wananchi. Kama wananchi wamedhamiria, kazi ya viongozi inakuwa ni kuchochea na kuunganisha nguvu za wananchi kufikia azima yao.
Tujifunze kutoka Afrika Kusini wiki hii. Jacob Zuma ‘amemnyang'anya chama’ Rais aliye madarakani, Thabo Mbeki, kwa sababu alinogewa, akasahau nguvu ya umma! Umma ukishaamua, kama umechoka na hauoni mtu anayefaa kutawala, unaweza kulichagua hata jiwe kuwa kiongozi!
Mbeki aliweka tumaini lake kwa vyombo vya dola na mashushushu wake. Alisahau kwamba hata mashushushu hawawezi kubadili nguvu ya umma uliokwishaamua.
Umma ukishasema ‘tumechoka,’ mjadala unakuwa umekwisha. Matendo yanafuata. Akipatikana kiongozi wa kuratibu matakwa ya umma, kazi inafanyika.
Wana ANC wamemuweka pembeni rais msomi aliyebobea, wakamchagua mtu ambaye ‘hakusoma hata darasa la saba.’ Kuna kitu wamekiona ndani mwake, ambacho Mbeki ama amekipoteza kwa kulewa madaraka, au hakuwa nacho kabisa, bali amejifunika mbwembwe za usomi na uzoefu.
Haya ni mapinduzi ya wananchi waliochoka, lakini wenye nguvu ajabu. Ni watu waliochoka, lakini wenye kutazama mbele bila kukata tamaa. Wanajua wanachotaka, wanapoona watawala hawakizingatii – wanawatimua.
Hii ni kengele kwa watawala wetu pia, kwamba tukiamua kuwanyang'anya chama na serikali na kuvirejesha mikononi mwa wakulima na wafanyakazi, hatutashindwa.
Lakini watawala wetu wakishaonja madaraka hawachelewi kulewa na kusahau au kupuuza kauli za wananchi. Itazame Kenya.
Ni nchi inayotupatia mafunzo mawili. Kwanza, imedhihirika kwamba ni vigumu kupata mabadiliko kwa kuwatumia watu wale wale walioshiriki kuunda mfumo ule ule tunaoupinga. Rais Mwai Kibaki amekuwa serikalini chini ya marais waliomtangulia, hayati Jomo Kenyatta na mstaafu Daniel arap Moi, kwa zaidi ya miaka 40.
Huyu si mtu anayeweza kuleta mabadiliko, kwa sababu amekuwa sehemu ya mfumo huu wanaoupinga sasa. Ni Kibaki huyu huyu, aliyepofushwa na madaraka, akiwa makamu wa rais miaka ya 1980, aliyewakejeli wapinzani waliokuwa wanadai mfumo wa vyama vingi.
Usomi wake na uzoefu wa kazi havikumpa uwezo wa kutambua kwamba mwisho wa KANU na mfumo wake unakaribia. Aliwakejeli wanaharakati na wapinzani akisema: “Hawa wanaota ndoto za mchana; ni sawa na watu wanaojaribu kuangusha mti kwa kutumia wembe.”
Miaka mitano iliyopita, yeye ndiye aliyekabidhiwa wembe huo huo, akakata mti huo huo ukaanguka! Hilo ndilo kosa walilofanya na funzo la kwanza wanalotupa Wakenya.
Kibaki amelelewa na kukulia mle mle. Ana mtandao wa kimasilahi na kimadaraka uliojengwa miaka nenda - rudi. Akili yake ni sehemu ya nguvu iliyounda mfumo mbovu wa utawala wa Kenya.
Haoni cha kubadili. Anafurahia utukufu. Ameshazoea adha, umaskini na kelele za wananchi maskini. Na kwa umri huo alionao, ni vigumu kumtarajia alete mabadiliko. Anaogopa mabadiliko kuliko anavyoogopa wananchi!
Funzo la pili ni hili la harakati za kumwondoa Kibaki huyo huyo. Wakenya sasa wamegundua kwamba walifanya makosa kumwamini na kumtanguliza Kibaki kwa kutazama tu usomi, uzoefu na umri wake.
Walichanganya mambo hayo na busara, wakasahau kwamba akishafika Ikulu ataona aibu kuwachukulia hatua wale wale alioshirikiana nao kuyajenga yale yale ambayo wananchi wanamtaka ayang’oe.
Tangu mwaka 2005, dunia imeshuhudia jinsi Wakenya walivyoamua kurekebisha makosa ya mwaka 2002. Walimpigia kengele rais, na wakaonyesha kwamba kama anafanya kinyume cha yale aliyowaahidi kwenye kampeni wana uwezo wa kumng’oa.
Walimtikisa akatikisika. Wakakataa mapendekezo ya katiba yake mbovu. Wakaungana na wapinzani kusema ‘rais ametuangusha. Aliyoahidi kwenye kampeni si anayofanya leo. Ametufanya wajinga. Hatuna dola, lakini tuna nguvu ambayo ilimweka pale. Hiyo hiyo tutaitumia kumwondoa.'
Kwa sababu ya kulewa madaraka, kuwapenda zaidi maswahiba wake kuliko taifa, rais alipuuza kengele waliyompigia; akapuuza kauli ya umma. Bado anadhani dola itamsaidia kuwalazimisha wamrejeshe madarakani.
Watu wale wale waliomuunga mkono mwaka 2002 wakisema hadharani: “Kibaki Tosha;” leo ndio wanaongoza harakati nchi nzima wakisema kwa nguvu ile ile; “Kibaki Toka.”
Yaliyompata Mbeki katika chama chake wiki iliyopita, yanaweza kumpata Kibaki katika serikali Alhamisi ijayo. Ni ishara kwamba nguvu ya umma inazidi mabavu ya rais aliye madarakani!
Sababu kubwa ni moja. Wote wawili wameshindwa kusoma alama za nyakati. Wamepuuza kauli za wananchi. Sasa wananchi wameweka woga pembeni. Wanasema imetosha.
Afrika haikuzoea kuona marais wakishindwa wakiwa madarakani, lakini nyakati zimebadilika. Kizazi hiki kina mtazamo tofauti, na kina nguvu ya ajabu itokanayo na shida zinazokikabili. Ni mapambano ya umaskini wa wananchi dhidi ya ulafi wa watawala unaowajengea dharau na jeuri.
Nimesikitika kwamba hata rais wetu, Kikwete, anayesifika kwa kuwa msikivu, anaanza kujifunza kwa Mbeki na Kibaki.
Wananchi wamempigia kengele; wanasema mawaziri wako ni wazembe. Yeye anasema ni wachapa kazi. Wanasema punguza ukubwa wa baraza au vunja uunde upya baraza lako la mawaziri; yeye anasema haoni haja. Wanamwambia mawaziri wako ni mzigo kwako na kwa taifa; yeye anasema hii ndiyo nguvu kazi ninayoitegemea.
Wananchi wanasema mrejeshe Gavana wa Benki Kuu, Daudi Ballali, ashitakiwe kwa tuhuma zinazomkabili, usimwache astaafu kimya kimya na kujificha nje ya nchi kwa kisingizio cha ugonjwa; yeye anasema hana habari kama gavana amestaafu.
Lakini wananchi hao hao wanahoji. Je, rais alisukumwa na nini kumteulia gavana msaidizi mara tu baada ya kutuhumiwa?
Zipo tetesi zinazunguka kwamba baadhi ya washauri wa rais wameshamtembelea Ballali huko aliko na kumshauri ‘asirejee nyumbani.’
Bahati mbaya wanaotuhumiwa kwa hili ni wale wale waliohusishwa na miradi ya utoroshaji wa pesa za umma kwa kutumia kampuni feki kama Deep Green katika kipindi cha uchaguzi mkuu.
Wananchi wamefika mahali wakasema hata imani yao kwa rais mwenyewe inaanza kupungua (kutoka asilimia 80, hadi 67, hadi 44 katika miaka miwili); yeye anasema hajashindwa na amefaulu.
Wananchi wanalalamikia ugumu wa maisha, bei za bidhaa muhimu zote zimepanda mara dufu, shilingi imeshuka thamani, kipato chao hakiongezeki; watawala wanasema uchumi ‘unapaa.’
Wananchi wanasema mlituahidi kutenda kazi kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya kwa kujitofautisha na serikali iliyotangulia. Mbona mmekwama na mnarudiarudia yale yale? Watawala wanasema ‘tupeni muda hadi 2010.’
Onyo: Mwaka 2010 hauko mbali. Wala hauji ghafla. Miaka miwili imepita. Bado miwili. Ule mmoja wa mwisho, kwa jinsi tunavyowajua CCM, utatumika kujiandalia uchaguzi mkuu.
Kwa hiyo, hesabu ya haraka haraka ambayo wananchi wanapaswa kufanya sasa ni kuzidisha mafanikio ya serikali ya sasa mara mbili – ingawa kasi ya utendaji inazidi kushuka, na ari ya watendaji inaporomoka pia.
Kama serikali inasema imefanikiwa kupambana na majambazi (kwa kutumia pikipiki); wananchi wanataka ipambane na mizizi ya ujambazi – na itambue kuwa majambazi wakubwa hawatumii silaha.
Serikali inasema imejishughulisha na kuinua soka; wananchi wanasema imejishughulisha na timu ya taifa, mmesahau ujenzi wa taasisi za michezo nchini na kujenga vitalu vya michezo yote.
Inasema imeijenga upya TAKUKURU; wananchi wanasema serikali imeshindwa kuiondoa ofisini mwa rais.
Mara kadhaa rais mwenyewe amekana kuingilia utendaji wa TAKUKURU, lakini sheria iko wazi kwamba yeye ndiye ‘bosi’ wa TAKUKURU! Yeye na watu wake wakituhumiwa watasafishwa kama ilivyotokea kwa Richmond. Na watu wanaamini kwamba rushwa zenyewe zinaliwa na wakubwa!
Zaidi ya hayo, baadhi ya wapambe wake wamekuwa wakisambaza ujumbe mara kwa mara kila TAKUKURU inapoonekana kuchukua hatua kadhaa; wao wanasema ‘rais ameagiza!’ wanajaribu kumjenga, wanamharibia!
Suala la Richmond (Dowans), mgongano wa maoni kuhusu ripoti ya TAKUKURU na Kamati ya Biashara na Uwekezaji ya Bunge, iliyosababisha kuundwa kwa Tume ya Bunge kuichunguza upya Richmond, ni suala jingine linalopunguza imani ya umma kwa serikali katika suala la rushwa.
Ndiyo maana watani wake wanasema rushwa imebaki Ikulu; ndiyo maana mafisadi wanatanua! Haya yote yanasemwa na wananchi hao hao. Rais msikivu anasikia, hasikilizi.
Kwa hiyo, wakati wananchi wanatambua kwamba yapo baadhi ya mambo yameshughulikiwa na serikali katika miaka miwili iliyopita, tatizo kubwa la serikali ya Kikwete ni kwamba imeshindwa kuvunja mfumo wa utawala iliourithi.
Ni jambo gumu, lakini liliahidiwa, na linawezekana. Au labda walifanya makosa yale yale ya Wakenya, kuwaamini watu wale wale kuleta mabadiliko wasiyoyaamini.
Kama ilivyo Kenya (na kwingine Afrika) tatizo letu ni mfumo. Unahitajika uongozi usio na huruma na mfumo uliopo, uuvunje vunje na kuunda mpya.
Kikwete na timu yake wana miaka miwili kutuhakikishia kwamba wanaweza hilo. Vinginevyo, wakiendelea kushughulika na vijimiradi vidogo vya kufurahisha wananchi kwa ajili ya kuombea kura, tutabaki pale pale alipotukuta au tutarudi nyuma zaidi.
Na siku wananchi watakapobaini kwamba Kikwete hasikilizi tena, ndiyo yale yale ya Mbeki na Kibaki, moto utakaowaka hautazimwa na nguvu zozote za dola hadi wananchi watakapopata jiwe la kuweka pale walipo watawala wa sasa. Lakini kwa nini tuchague jiwe?
http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=10980
No comments:
Post a Comment